Follow by Email

Friday, April 28, 2017

Waziri Mahiga ahitimisha ziara ya kikazi Jamhuri ya Korea kwa mafanikio

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Yun Byung-se. Mhe. Mahiga alikuwa nchini humo kwa ziara ya kikazi ikiwa pia ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea.
=====================================================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alifanya ziara ya kikazi jijini Seoul, Jamhuri ya Korea tarehe 24 Aprili 2017 kwa mwaliko kutoka kwa Mhe. Yun Byung-se, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea. Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea mwaka 1992.

Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Yun Byung-se ambapo Waziri Mahiga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kumpatia mwaliko wa kutembelea taifa hilo hususan wakati huu inapoadhimishwa jubilee ya miaka 25. Mhe. Mahiga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kimkakati  katika uwekezaji kwa kipindi cha kuanzia 2016 -2020.

Kwa kipindi cha miaka 25, Serikali ya Korea imeisaidia Tanzania kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo Ujenzi wa Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi unaojumuisha madaraja matatu yenye jumla ya urefu wa meta 275  pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 48; Ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Mloganzila yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 600 imejengwa na kufungwa vifaa tiba vya kisasa vya digitali, vinavyotumia zaidi teknolojia ya Tehama zikiwemo mashine za X-ray, MRI, CT-Scan, mashine maalum kwa ajili ya kupimia magonjwa ya wanawake. 

Vilevile, Ujenzi wa Hospitali ya mama na mtoto Chanika yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 160 inatarajiwa kufunguliwa siku za karibuni.Aidha, Watanzania zaidi ya 1000 wamenufaika kwa kupata ufadhili wa kusoma katika vyuo mbalimbali vya Jamhuri ya Korea.

Waziri Mahiga pia alikutana na baadhi ya Wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Korea ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania mathalani ujenzi wa Reli ya Kati katika viwango vya kimataifa; uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme; ujenzi wa maeneo ya viwanda; na huduma ya kutoa ushauri katika miradi mikubwa.

Aidha, Mhe. Waziri aliwahakikishia wawakilishi wa  makampuni ya Jamhuri ya Korea kuwa, Tanzania imeboresha mazingira ya uwekezaji na biashara pamoja na taasisi muhimu zinazotoa huduma mbalimbali katika sekta hiyo. 

Wakati huo huo, Mhe. Waziri Mahiga alitumia fursa hiyo kukutana na Balozi Sul Kyung-hoon Makamu wa Rais wa KOICA ambapo aliishukuru Taasisi hiyo kwa kuipatia zaidi misaada Tanzania kwa uwazi na bila ya masharti yeyote. Pia aliipongeza KOICA kwa kushirikisha jamii kuanzia wakati wa ubunifu wa mradi hadi kufikia utekelezaji pamoja na usimamizi. KOICA wameombwa kuongeza maeneo ya misaada na kujumuisha maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya maji na nishati ya umeme wa jua, upepo na maji kwa ajili ya kusaidia maeneo ya vijijini. Aidha, Mhe. Waziri Mahiga alishauri KOICA kuangalia uwezekeno wa kuanzisha vituo vya kilimo cha kisasa, vituo vya kufugia na vituo vya kufundisha ujasiriamali ili jamii kubwa ya Watanzania iweze kunufaika.

Katika jitihada za kutafuta washirika kwa ajili ya kusaidia kuboresha Chuo cha Diplomasia, Mhe. Waziri akiwa Seoul alitembelea Chuo cha Taifa cha Diplomasia cha Jamhuri ya Korea na kufanya mazungumzo na Balozi Paik Ji-ah, Kaimu Mkuu wa Chuo. Lengo kuu lilikuwa kujifunza uendeshaji wa Chuo, mitaala iliyoandaliwa kutoa masomo, walengwa wa masomo hayo, aina ya wakufunzi, lugha zinazotumika kufundishia, utaratibu wa kuandaa wanadiplomasia na mifumo ya chuo hicho.

Vilevile kabla ya kuhitimisha ziara yake, Mhe. Waziri alikutana na Jumuiya ya Watanzania waishio Jamhuri ya Korea ambapo aliwahimiza kuheshimu Sheria na Taratibu za nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuleta utaalam utakaosaidia kuiendeleza Tanzania.

Aidha, akizungumza  na Watanzania hao ambao wengi wao ni wanafunzi, Mhe. Waziri aliwasihi kuzingatia masomo ili kufikia malengo waliyojiwekea na kuleta faida kwa familia zao na taifa kwa ujumla. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri aliwahakikishia Wanajumuiya hao kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kufungua Ubalozi wa Tanzania jijini Seoul na kuwaomba kutoa ushirikiano kwa Balozi wa kwanza wa Tanzania katika nchi hiyo. 

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 28 Aprili, 2017

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana na Mkurugenzi wa IFAD Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba akizungumza na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo-IFAD wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bw. Sana Jatta alipofika Wizarani tarehe 28 Aprili, 2017. Pamoja na mambo mengine walizungumzia namna ya kuendeleza miradi ya kilimo na ufugaji hapa nchini kwa ajili ya kujihakikishia usalama wa chakula na lishe bora kwa maendeleo.
Sehemu ya ujumbe kutoka Ofisi za IFAD hapa nchini alioambatana nao Bw. Jatta. Kulia ni Bw. Francisco Pichon, Mwakilishi na Mkurugenzi wa IFAD nchini akiwa na Bi. Mwatima Juma Afisa Miradi Mwandamizi wa IFAD nchini.
Bw. Jatta nae akimweleza jambo Mhe. Dkt. Susan wakati wa mazungumzo yao.


Sehemu ya ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Jestas Nyamanga, Bi. Eva Ng'itu, Afisa Mambo ya Nje na Bw. Charles Faini, Msaidizi wa Naibu Waziri.
Mhe. Dkt. Kolimba katika picha ya pamoja na wageni wake.

Thursday, April 27, 2017

Wabunge wa EALA watoa elimu ya fursa za Mtangano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Wafanyabiashara wa Dodoma

Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Adam Kimbisa akizungumza na wajumbe kwenye semina ya kutoa elimu ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sambamba na kuhamasisha fursa zinazotokana na mtangamano huo kwa wafanyabiasahara wa mjini Dodoma. Semina hiyo inayohusisha wafanyabiashara na makundi mbalimbali katika jamii pamoja na mambo mengine inalenga kuongeza urari wa biashara wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; semina hii itaendelea kesho Mjini Dodoma.
Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Stephen Mbundi akifafanua jambo kwenye semina hiyo. Bw. Mbundi alitumia fursa hiyo kutolea ufafanuzi masuala mbalimbali yaliyoulizwa na wafanyabiashara na wadau wengine walioshiriki semina hiyo.

Mmoja wa wajumbe akizungumza katika semina hiyo

Semina ikiendelea

Mmoja wa wajumbe kutoka kundi la wafanyabiashara akizungumza


Mwenyekiti wa Wabunge wa Tanzania wanaowakilisha Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Makongoro Nyerere (kulia) akikabidhi bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwakilishi wa wafanyabiashara mara baada ya semina

Uingereza na Tanzania kushirikiana katika uboreshaji wa huduma za jamii.

Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. Sarah Cooke alipomtembelea leo katika ofisi za Wizara. Katika mzungumzo yao Mhe. Kolimba alieleza nia ya Serikali ya Tanzania katika kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Uingereza sambamba na kuzungumzia miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali yake katika kuwaletea maendeleo na kuboresha maisha ya watanzania.
 Mhe. Sarah akimweleza Mhe. Kolimba malengo ya Serikali ya Uingereza katika kuimarisha maeneo ya ushirikiano hususan katika sekta ya kilimo, elimu, afya sambamba na ujenzi wa miundombinu.

Mazungumzo yakiendelea, kulia ni maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje wakifuatilia mazungumzo hayo.

Picha ya pamoja.

Tuesday, April 25, 2017

Serikali yamuondoa Mkurugenzi wa UNDP nchini


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali yamuondoa Mkurugenzi wa UNDP nchini 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeliagiza Shirika la Umoja wa Mataifa la Programu ya Maendeleo (United Nations Development Programs – UNDP) kwa upande wa Tanzania kumuondoa nchini Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi Awa Dabo.
Serikali ilifikia uamuzi huo kutokana na  Bi Dabo kutokuwa na maelewano mazuri na baadhi ya Watumishi wenzake na Menejimenti ya Shirika hilo, hivyo kupelekea kuzoretesha utendaji wa shirika hilo nchini na kupunguza kasi ya kuleta maendeleo kwa Watanzania endapo hatua za haraka zisingechukuliwa.
Baada ya kuthibitishiwa kuondoka nchini, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imetoa rai kwa UNDP kuwakumbusha Watumishi wake kuwa kipaumbele chao ni kufanya kazi na Serikali ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano na Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo yamefafanuliwa katika Agenda ya Mwaka 2030.  

Mwisho.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasili ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma, 25 Aprili 2017.


Saturday, April 22, 2017

Naibu Waziri afanya mazungumzo na Mabalozi Wateule

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba amekutana na kufanya mazunguzo na Mabalozi Wateule wanaoenda kuiwakilisha Tanzania maeneo mbalimbali Duniani.Mazungumzo hayo yaliyofanyika ofisini kwake Makao Makuu ya Nchi mjini Dodoma, yalijikita katika kujadili namna bora ya kuiwakilisha Tanzania ughaibuni kwa kuzingatia sera ya nchi ya mambo ya nje,  kwa lengo la kuboresha mahusiano ya Kidiplomasia baina ya Tanzania na nchi hizo, na kwa kuzingatia maslahi mapana ya kiuchumi ya nchi yetu ikiwemo kutangaza shughuli za utalii zinazopatikana nchini.

Naibu Waziri Mhe. Dkt. Susan Kolimba akisisitiza jambo

Balozi Mteule Baraka H. Luvanda akichangia jambo wakati wa mazungumzo.

Punde baada ya mazungumzo na Mhe. Naibu Waziri, Mabalozi walikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 

Katibu Mkuu Wizara Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt.Aziz P Mlima akiongea na Mabalozi ofisini kwake mjini Dodoma


Mazunguzo yakiendelea

Thursday, April 20, 2017

Wizara yajidhatiti kukarabati miundombinu ya Ofisi za Balozi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba akijibu swali la Mhe. Raisa Adallah Musa Bungeni katika kipindi cha maswali na majibu mapema leo asubuhi, amesema kuwa Wizara kwa kutumia bajeti ya maendeleo ya Serikali na vyanzo vingine vya mapato inaendelea kutekeleza mkakati wa kurekebisha na kuboresha miundombinu ya Ofisi za Balozi na makazi ya watumishi wa ubalozini katika maeneo mbalimbali yenye uwakilishi Duniani. Mkakati huu unahusisha ukarabati wa majengo yaliyopo, ujenzi wa majengo mapya, sambamba na ununuzi wa majengo mapya. Mkakati huu unaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha ujao 2017/2018.  

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba akijibu maswali kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge katika  Kikao cha Bunge kwenye kipindi cha maswali na majibu 

Thursday, April 13, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARITAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Watanzania waliokuwa wanashikiliwa nchini Malawi waachiwa huru

Mahakama Kuu ya Mzuzu nchini Malawi jana tarehe 12 Aprili 2017 iliwaachia huru Watanzania wanane waliokuwa wanashikiliwa nchini humo kwa kosa la kuingia kinyume cha sheria kwenye mgodi wa urani wa Kayerekera. 

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Mzuzu, Bw. Texious Masoamphambe alitoa hukumu ya kifungo cha mwezi mmoja kwa kosa la kuingia kinyume cha sheria kwenye mgodi wa urani wa Kayerekera (trespass) na kifungo cha miezi mitatu kwa kosa la kufanya ujasusi (reconnaissance).

Makosa hayo mawili, kifungo chake kinakwenda pamoja na kwa mujibu wa Hakimu huyo watuhumiwa tayari wameshatumikia kifungo hicho na kuamuru waachiliwe huru. Aidha, Hakimu aliamuru Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Ndani kuhakikisha kuwa Watanzania hao wanasafirishwa na kurejeshwa makwao haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, Watanzania hao wamesafirishwa leo tarehe 13 Aprili 2017, kutoka Mzuzu hadi Mpaka wa Songwe/Kasumulu kati ya Tanzania na Malawi.  

Watanzania hao ambao ni Walasa Mwasangu, 30, Binto Materinus, 32, Ashura Yasiri, 63, Christian Msoli, 38, Layinali Kumba, 47, Maliyu Mkobe, Gilbert Mahumdi, 32, na Martin Jodomusole, 25 walikuwa wamekamatwa na kushikiliwa na vyombo vya usalama vya Malawi tokea tarehe 20 Desemba 2016.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 13 Aprili  2017.